Header Ads

Mh.Magufuli asema atahakikisha wawekezaji migodini wanachangia maendeleo ya wananchi.


Serikali ya awamu ya tano ya chama cha mapinduzi CCM imewahakikishia wananchi wa mkoa wa Mara ambao sehemu kubwa umezungukwa na migodi ya madini kuwa itahakikisha wawekezaji kwenye migodi hiyo wanachangia maendeleo ya wananchi wa maeneo husika sanjari na kukuza pato la taifa kupitia maliasili zilizopo nchini endapo wananchi wataipa ridhaa ya kuliongoza taifa.
Mgombea wa kiti cha urais kupitia CCM Dr John Pombe Magufuli ambaye amefanya mikutano minne katika maeneo ya Nyamongo, Tarime, Rorya, Musoma vijijini na hatimae Musoma mjini kwenye uwanja wa Mkendo ambapo ameendelea kusisitiza kauli yake ya maendeleo hayana chama na kuahidi kutatua kero mbalimbali kulingana na maeneo alikopita na kusisitiza kuwa serikali yake haitakuwa na msalie mtume kwa mafisadi, wezi, na wazembe ili mwananchi wa kawaida aweze kupata faraja ya kuwa mtanzania.
Kuhusiana na suala la maliasili za taifa hususani madini Dr Magufuli amesema serikali yake inawakaribisha wawekezaji wa nje na wa ndani kwa lengo la kusaidia kupunguza tatizo la ajira na kukuza uchumi lakini kamwe hatakubali Tanzania kugeuzwa shamba la bibi.
Dr Magufuli anahitimisha ziara yake mkoani Mara ambapo aliwasili akitokea mkoani Tanga na kuzuru kaburi la baba wa taifa hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere na baadae kukabidhiwa na wazee wa eneo la Butiama kifimbo kama cha baba wa taifa kama ishara ya kiongozi ama mtawala anayekubalika na anatarajiwa kuendelea na ziara yake mkoani Simiyu jumamosi sept 12.

No comments

Powered by Blogger.