KISHIMBA AAHIDI NEEMA KAHAMA
Na Chibura Makorongo, Kahama
MGOMBEA ubunge wa jimbo la
Kahama mkoani Shinyanga, Jumanne Kishimba (CCM), amesema iwapo atachaguliwa
kuwa mbunge wa jimbo hilo, atahakikisha hospitali ya wilaya hiyo inapandishwa
hadhi na kuwa ya rufani.
Pia, alisema atashughulikia kwa
haraka uanzishwaji wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Kahama.
Kishimba alitoa ahadi hiyo juzi alipokuwa
akiwahutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Kahama na vitongoji vyake, katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CDT mjini hapa, kwa ajili ya
kampeni za kuomba kura kwa wananchi na kunadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Aliwaomba wakazi wa jimbo la Kahama,
kuhakikisha kuwa Oktoba 25, mwaka huu, wanampigia kura za kishindo ili aweze
kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa vile amedhamiria kwa dhati kushirikiana nao
katika suala zima la maendeleo.
Akifafanua kuhusu ahadi ya
kuipandisha hadhi hospitali ya sasa ya serikali wilayani humo, alisema wilaya
hiyo hivi sasa ina ongezeko kubwa la wakazi huku wengine wakitoka mikoa jirani,
ambao wanategemea huduma za matibabu kutoka katika hospitali hiyo na hivyo
kuzidiwa na idadi ya wagonjwa.
“Ndugu zangu wakazi wa Kahama,
tumekutana katika mkutano huu kwa lengo la kuwaomba kura kutoka kwenu, naomba
mnichague niweze kuwa mwakilishi wenu bungeni, na moja ya mambo muhimu
ninayowaahidi iwapo nitachaguliwa ni kupigania hospitali yetu hii iweze
kupandishwa hadhi,” alisema.
Kuhusu kuanzishwa kwa Baraza la
Ardhi la Wilaya ya Kahama, alisema pia itakuwa ni moja ya vipaumbele vyake
na kwamba kuanzishwa kwa baraza hilo ambalo tayari mamlaka husika zilisharidhia
uanzishwaji wake, utasaidia kupunguza migogoro mingi ya ardhi iliyopo kwa sasa.
“Kwa mujibu wa takwimu zilizopo,
asilimia 75 ya migogoro yote ya ardhi inayofikishwa katika Baraza la Ardhi
mkoani Shinyanga, inatoka wilaya ya Kahama, sasa ni vizuri tukawa na baraza
letu wenyewe ili kuwapunguzia wananchi gharama za kwenda mkoani kila mara,”
alisema.
Mwenyekiti wa CCM wilayani Kahama,
Mabala Mlolwa, aliwaomba wakazi wa wilaya hiyo wasifanye makosa Oktoba
25, mwaka huu, na wahakikishe wanawapigia kura wagombea wote wa CCM, kuanzia
rais, mbunge na madiwani waliosimamishwa na Chama.
No comments